Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wametakiwa kuwa mabalozi wa kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani kipindi chote cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili shughuli za biashara zifanyike kwa usalama huku wakilipa kodi kwa uaminifu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa tamasha la Gulio la Kariakoo (Kariakoo Festival) leo (15 Agosti 2025) Dar es Salaam lenye lengo la kutangaza fursa za biashara na masoko yaliyopo nchini.
“Tarehe 29 Oktoba mwaka huu tutakuwa na Uchaguzi Mkuu, niwaalike wafanyabiashara wa Kariakoo kuwa mabalozi wa amani ili shughuli za kibiashara katika eneo lote la Kariakoo na Tanzania kwa ujumla zifanyike kwa amani na utulivu” alisisitiza Dkt. Jafo.
Naye Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Yusuph Mwenda alisisitiza kuwa iko tayari kuendelea kuwasikiliza wafanyabiashara na kutatua kero zao ili walipe kodi kwa mujibu wa Sheria.
Mwenda aliongeza kuwataka wafanyabiashara kote nchini kuendelea kulipa kodi kwa uaminifu ili Serikali ipate mapato ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Abdulkarim alieleza kuwa tamasha hilo ni fursa nzuri kwa wadau wa Soko la Kariakoo kuwafikia wateja ndani na nje ya nchi.
CPA Abdulkarim aliongeza kusema, Shirika lipo kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea kurejesha wafanyabiashara ndani ya Soko baada ya Serikali kukamilisha ujenzi na ukarabati wa soko ambapo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha Bilioni 28.
Mwisho.
General Manager, Kariakoo Markets Corporation, Nyamwezi/Tandamti Street,
Postal Address: P. O. Box 15789 Dar es Salaam, Tanzania
Telephone: +255 22 2180678
Mobile:
Email: info@kariakoomarket.co.tz
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.