KARIAKOO KUSAJILI TAARIFA ZA WAFANYA BIASHARA WAKE KATIKA KANZI DATA MAALUM
Shirika la Masoko ya Kariakoo limekamilisha maandalizi ya kuanzisha kanzi data maalum ya wafanyabiashara wa soko la Kariakoo, kanzi data ambayo itakuwa na taarifa kamili ya mfanyabiashara ikionesha majina kamili, aina ya biashara, namba ya eneo la biashara, ukubwa wa eneo namba ya mlipakodi na namba ya kitambulisho cha taifa, malipo anayostahili kulipa pamoja na kiasi kilicholipwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo CPA.Ashraph Abdulkarim, kuandaliwa kwa kazi data hiyo kunatokana na maboresho ya mifumo ya tehama ambayo inawezesha soko hilo kutunza taarifa zake kwa njia ya kidigitali jambo ambalo ni muhimu katika kuzuia upotevu wa nyaraka na taarifa.
“Kanzi data hii italiwezesha shirika kupata taarifa sahihi za wafanyabiashara wake kwa wakati ambapo taarifa hizi huishi kwa muda mrefu na pia haziwezi kuathiriwa na changamoto ya mvua au kuharibika kwa namna yeyote ile” amebainisha CPA. Ashraph Abdulkarim
CPA. Abdulkarim ameongeza kuwa uwepo wa kanzi data hiyo ni mwendelezo wa mikakati ya shirika hilo kuendelea kusimamia ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya shirika hilo ili soko la Kariakoo liendelee kuzalisha kwa tija na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukarabati na Kujenga upya soko hilo la Kimataifa hapa nchini.
Ikumbukwe kuwa Soko la Kariakoo liliungua mwaka 2021, ambapo serikali ilianza ukarabati na ujenzi wa soko hilo upya mwaka 2022 ambapo mpaka sasa ukarabati na ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 99 na soko hilo litafunguliwa hivi karibuni.
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.