Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa lililokuwa soko dogo na ukarabati wa soko kuu la Kariakoo lilioungua Julai 2021 umetajwa kuwa moja ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita tangu ilipoingia madarakani miaka minne iliyopita.
Mafanikio hayo yameleezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Hawa Ghasia Machi 14,2025 alipozungumza na kituo cha Televisheni cha ZBC jijini Dar es Salaam kuelezea maandalizi ya kurejesha shughuli katika Soko la Kariakoo.
Katika mazungumzo hayo yaliyorushwa mubashara kupitia kipindi cha Asubuhi Njema, Ghasia alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi Bilioni 28.03 mwaka 2022 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa kimkakati ambao umekamilika mwaka huu.
“Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti, na Watumishi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo tunatoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya uongozi wake wenye mafanikio makubwa kwa taifa letu” alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi.
Ghasia aliongeza kusema chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia, Soko la Kariakoo limepata mageuzi makubwa, limejengwa upya na kufanyiwa ukarabati wa kisasa, ambapo litawanufaisha wafanyabiashara zaidi ya 2000 na ajira zaidi ya 4000 zikitarajia kupatikana.
Alipoulizwa kuhusu lini Soko la Kariakoo litarejesha shughuli zake, Ghasia alitaja mwezi Aprili mwaka huu kazi ya kuwapanga wafanyabiashara kwenye maeneo ndani ya soko itakamilika na hivyo kufanya soko lianze kazi kwa muda wa saa 24.
General Manager, Kariakoo Markets Corporation, Nyamwezi/Tandamti Street,
Postal Address: P. O. Box 15789 Dar es Salaam, Tanzania
Telephone: +255 22 2180678
Mobile:
Email: info@kariakoomarket.co.tz
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.