Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeridhishwa na ujenzi unaoendelea wa Mradi wa Soko la Kariakoo jijini Dar es salaam.
Akizungumza mara baada ya ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Mradi wa Soko la Kariakoo ( tarehe 21 Februari, 2025) pamoja na kujionea eneo lilipotokea tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Florent Kyombo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ilivyopambana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha inaokoa watu na mali wakati yalipotokea maafa nchini.
Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ujenzi wa mradi wa soko la Kariakoo ni hatua nzuri ambayo itasaidia wafanyabiashara na wengine wanaopata huduma katika eneo hilo kufanya shughuli zao katika eneo rafiki na salama.
Akizungumza kuhusu jengo lililoporomoka katika eneo la Kariakoo alisema Serikali imeendelea kuratibu vyema masuala ya menejimenti ya maafa nchini kwa kuchukua hatua za haraka katika kunusuru uhai na mali za watu wake pindi maafa yanapotokea.
“Tunaendelea kuishukuru na kuipongeza Serikali kupitia Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa na moyo wa kujali aliouonesha wakati wote tulipopatwa na haya maafa hadi sasa Serikali inapoendelea kuimarisha miundombinu na kurejesha hali,” Amesema Mhe. Kyombo.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa uamuzi wake wa kutembelea na kujionea athari zilizotokana na kuanguka kwa ghorofa hilo na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi wa Soko la Kariakoo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Mary Maridadi alieza kuwa taratibu za kuwarejesha waliokuwa wafanyabiashara 1,520 waliokidhi sifa na vigezo vya uhakiki zinaendelea kuratibiwa.
General Manager, Kariakoo Markets Corporation, Nyamwezi/Tandamti Street,
Postal Address: P. O. Box 15789 Dar es Salaam, Tanzania
Telephone: +255 22 2180678
Mobile:
Email: info@kariakoomarket.co.tz
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.