JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Dar es Salaam, 29 Januari,2025
Ndugu wanahabari
Nimewaita hapa leo kuzungumza nanyi juu ya hatua zinazoendelea kwenye maandalizi ya kurejesha shughuli za biashara kwenye soko la Kariakoo. Itakumbukwa kuwa soko la Kariakoo lilipata ajali ya moto tarehe 10 Julai 2021 na kusababisha wafanyabiashara kuondolewa na shughuli kusimama.
Tangu kipindi hicho serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko hilo ulioanza mwezi Januari 2022 na sasa umefikia hatua za kukamilika. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 28.03 zilizotumika kufanikisha mradi huu wa kimmkakati wenye nia ya kulifanya Soko la Kariakoo kuwa la kimataifa.
Ndugu wanahabari
Tarehe 27 Januari 2025 Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika ilikutana hapa Dar es Salaam ambapo pamoja na agenda zingine ilijadili na kuazimia kuwa kazi ya kuwarejesha wafanyabiashara kwenye soko la Kariakoo ianze mapema mwezi Februari mwaka huu. Uamuzi huu wa Bodi ya Wakurugenzi unafuatia kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa soko sambamba na kukamilika kwa kazi ya uhakiki wa waliokuwa wafanyabiashara kwenye soko hilo uliofanywa na Timu Maalum iliyoundwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikijumuisha wawakilishi wa Wafanyabiashara, Menejimenti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo na vyomba vya Usalama.
Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika ninachukua fursa hii kuwajulisha wananchi na wafanyabiashara kuwa Soko la Kariakoo litarejesha shughuli zake kuanzia mwezi Februari, 2025. Menejimenti inaratibu kazi ya kutangaza majina ya waliokuwa wafanyabiashara kwenye Soko hilo ambao wamekidhi vigezo na sifa za kurejeshwa baada ya uhakiki. Uhakiki uliofanywa umebaini jumla ya wafanyabiashara1,520 wanaotarajiwa kurejeshwa sokoni. Majina na fomu ya kujiunga vitatangazwa kwa umma kupitia vyombo vya habari ikiwemo tovuti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo na tovuti ya OR - TAMISEMI.
Hivyo nitoe wito kwa wafanyabiashara na wananchi kuwa Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa kushirikiana na mamlaka zingine za Serikali ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam itaendelea kutoa taarifa kwa wananchi juu ya utaratibu utakaotumika kipindi chote cha kuelekea ufunguzi wa soko la Kariakoo.
Ndugu wanahabari
Natoa wito kwa Wafanyabiashara wote wenye madeni kulipa madeni yao kabla ya kurejea Sokoni. Takwimu zetu zinaonyesha jumla ya wafanyabiashara 366 wanadaiwa na Shirika Shilingi 358,571,106.85.
Wafanyabiashara na wananchi wote wenye sifa za kuingia sokoni watatangaziwa utaratibu utakaotumika, hivyo Shirika linawataka kuendelea kuwa na subira wakati Mamlaka zikikamilisha taratibu.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Hawa Abdurahman Ghasia
MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI
S.L.P 15789, DAR ES SALAAM
Barua-pepe : info@kariakoomarket.co.tz Tovuti : www.kariakoomarket.co.tz
General Manager, Kariakoo Markets Corporation, Nyamwezi/Tandamti Street,
Postal Address: P. O. Box 15789 Dar es Salaam, Tanzania
Telephone: +255 22 2180678
Mobile:
Email: info@kariakoomarket.co.tz
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.