DC MPOGOLO ATINGA KARIAKOO USIKU, BARABARA ZAFUNGUKA.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amesema Serikali ya wilaya hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara, machinga na waendesha bodaboda pamoja na wadau wengine wa Kariakoo kuhusu umuhimu wa kuacha wazi na kuwezesha kupitika kwa barabara zinazoingia na kutoka soko la Kariakoo.
Mhe. Mpogolo ametoa kauli hiyo alipofanya ziara eneo la kariakoo majira ya usiku ili kujionea utekelezaji wa mpango wa kufungua barabara Kariakoo huku akiwa ameambatana na Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, viongozi wa Juimuiya ya Wafanyabiashara, viongozi wa Machinga pamoja na viongozi wa boda boda na maguta.
Mhe. Mpogole amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaokaidi agizo la kufungua barabara, kwakuwa watu wengi wameitikia agizo hilo chanya na kuipongeza serikali kwa uamuzi huo kwakuwa sasa baadhi ya barabara zinapitika na kuondoa usumbufu kwa wadau mbalimbali wanaofika Kariakoo kwa shughuli mbalimbali.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA. Ashraph Abdulkarim ameishukuru Serikali ya Mkoa, Wilaya pamoja na Uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kwa namna ilivyoshughulikia zoezi la kufungua barabara zinazoingia na kutoka Soko Kuu la Kariakoo kwa weledi mkubwa na sasa zinapitika bila usumbufu wowote.
Naye, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Elihuruma Mabelya amesema zoezi la kufungua njia za kutoka na kuingia Kariakoo lilikuwa ni shirikishi na lilikuwa na lengo la kulinda mtaji ambao umewekwa na serikali Soko Kuu la Kariakoo na kufanya soko hilo kuwa taswira njema kwa watu kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa ufanisi.
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.