MALORI YA BIASHARA YA JUMLA RUKSA SHIMONI KARIAKOO, MSAMAHA WA USHURU KWA WIKI MBILI.
Uongozi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo umeruhusu magari ya mizigo kuingiza vyakula katika katika Soko Kuu la Kariakoo (shimoni) ili kuwarahisisha huduma za upatikanaji wa vyakula vya jumla kwa wafanyabiashara wa soko hilo la kimataifa na kongwe nchini na kutoa msamaha wa ushuru kwa kipindi cha wiki mbili.
Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja Mkuu wa Shirika hilo, CPA Ashraph Abdulkarim wakati wa zoezi usafi ikiwa ni maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar, kufuatia maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo wa kuruhusu magari hayo kuingia sokoni hapo.
CPA. Abdulkarim ameongeza kuwa uamuzi wa magari kuingia sokoni hapo kutatanua wigo wa upatikanaji wa bidhaa za chakula sokoni hapo kupatikana kwa jumla, hivyo kusaidia wafanyabiashara wa masoko mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha, magari yatakayoruhusiwa kuingia sokoni hapo mchana ni yale ambayo yapo chini ya tani tano tu ambapo yale ambayo ni zaidi ya ujazo huo yataingia sokoni hapo majira ya usiku ili kutoathiri shughuli zingine za wafanyabiashara ndani ya eneo la Kariakoo.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano hufanyika Aprili 26 kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Miaka 62 ya Muungano: Amani, Umoja, na Mshikamano ni Msingi wa Maendeleo Endelevu”
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.