WAFANYABIASHARA KARIAKOO WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KUZINGATIA USAFI.
Shirika la Masoko ya karikoo limeendelea kuwakumbusha wafanyabishara wa Soko Kuu la Kariakoo umuhimu wa kutunza mazingira ya soko na kuzingatia usafi binafsi wa wafanyabiashara ili kulinda afya zao na wateja kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Afisa Afya Mazingira Bw. Sunday Ringo wakati akitoa elimu kwa wafanyabiashara hao, elimu ambayo imelenga kuongeza uelewa kuhusu masuala ya usafi ili kuepuka magonjwa ya kuambukiza ambayo yanaweza kusababishwa na kutozingatia kanuni za afya na usafi.
Bw. Ringo ameongeza kuwa Soko Kuu la Kariakoo ni la kimataifa hivyo ni lazima shughuli zinazofanyika sokoni hapo zifanyike katika mazingira ya usafi ambao unakidhi kanuni na miongozo ya kimataifa na hivyo kuendelea kuwa kivutio ndani na nje ya nchi.
Bw. Ringo amesisitiza wafanyabiashara hao husani wale wanaojihusisha na biashara ya kukuna nazi pamoja na wale wauzaji wa mboga kuvaa gloves maalum ambazo zitawafanya wafanyabiashara hao wasishike mboga hizo moja kwa moja.
Kwa upande wake Afisa Afya Mazingira Masaidizi Bi Bahati Godi aliwasihi wafanyabiashara kuendelea kuzingatia kanunuzi zote za afya na usafi ili kuweza kulinda afya zao na afya za wateja wote wanaolitumia soko kuu la Kariakoo.
Wafanyabiashara hao wameushukuru uongozi wa Soko hilo kwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kuahidi kufuata maelekezo waliyopata kutoka kwa wataalam na kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara wengine ambao hakuwepo katika zoezi la kutoa elimu.
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.