Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea kutatua kero za wafanyakazi nchini imefanikiwa kutoa shilingi Milioni Mia Tatu na Sita kwa ajili ya kulipa madeni ya waliokuwa watumishi wa Soko la Kariakoo.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo Hawa Ghasia wakati wa kikao cha Kumi cha Bodi hiyo kilichofanyika ukumbi wa Arnautoglo Dar es Salaam jana Aprili 17,2025.
“Rais Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha waliokuwa wafanyakazi wa Shirika letu na kutupatia shilingi milioni 306 kulipa madeni. Nataka kuona ifikapo mwisho mwa wiki hii fedha zimelipwa kwa walengwa kwani wamesubiri kipindi kirefu” aliagiza Ghasia.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim alisema Shirika limepokea fedha hizo toka Hazina kufuatia maombi ya siku nyingi.
CPA Abdulkarim alibainisha kuwa fedha hizo zitalipwa kwa waliokuwa watumishi wa Shirika ambao kwa sasa wamestaafu ambapo umakini utazingatiwa ili haki itendeke.
Akitoa takwimu za wanaostahili kulipwa, Meneja wa Fedha wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Semeni Yamawe alisema jumla ya wastaafu kumi na tisa (19), pia wapo warithi ambao ndugu zao walikuwa watumishi lakini sasa ni marehemu pamoja na wastaafu ambao walishinda kesi mahakamani.
Katika hatua nyingine, Bodi ya Wakurugenzi imeelekeza Menejimenti ya Shirika kusimamia kikamilifu mpango kazi wa kuelekea ufunguzi wa soko la Kariakoo ikiwemo kuwapanga wafanyabiashara kwenye maeneo na kutoa mikataba ili shughuli zirejee sokoni.
Soko la Kariakoo linatarajia kurejesha shughuli zake hivi karibuni baada ya kukamilika kwa mradi wa kimkakati wa ujenzi wa soko jipya lenye sakafu nane na ukarabati wa lililokuwa soko kuu uliogharimu shilingi Bilioni 28.03 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Mwisho.
General Manager, Kariakoo Markets Corporation, Nyamwezi/Tandamti Street,
Postal Address: P. O. Box 15789 Dar es Salaam, Tanzania
Telephone: +255 22 2180678
Mobile:
Email: info@kariakoomarket.co.tz
Copyright ©2024 Shirika la Masoko ya Kariakoo . All rights reserved.